Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano Iraq yawatimua watu zaidi Anbar

Mapigano Iraq yawatimua watu zaidi Anbar

Watu wapatao 180,000 wamelazimika kuhama makwao katika jimbo la Anbar nchini Iraq, kufuatia mapigano makali katika maeneo ya Heet na Ramadi baina ya vikosi vya usalama vya serikali ya Iraq na wanamgambo wanaotaka kuweka dola la Uislamu wenye msimamo mkali, ISIL katika siku chache zilizopita. Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Dharura, OCHA, imesema kuwa makadirio ya awali yanaonyesha kuwa asilimia 75 ya wakazi wa Heet sasa wameukimbia mji huo uliokuwa na wakazi 300,000.

OCHA imesema Maelfu ya wanaume, wanawake na watoto wanaripotiwa kuwa safarini bado, wengi wao wakiwa kwenye malori barabarani, wakihitaji kwa dharura usaidizi wa kunusuru uhai wao, kama vile chakula, maji na makazi.

Baadhi ya watu waliolazimika kuhama makwao wamesalia kwenye jimbo la Anbar, huku wengine wakikimbilia Kerbala na Baghdad. Kabla ya wimbi hili jipya la wakimbizi, tayari mji wa Heet ulikuwa na wakimbizi wa ndani wapatao 100,000, kwa hiyo kuna uwezekano wengine sasa wanajikuta wakikimbia kwa mara ya tatu au hata nne.

Umoja wa Mataifa umeanza kuwafikia wakimbizi hao kwa kutoa chakula cha watu 30,000 kupitia shirika la Mpango wa Chakula, WFP, vifaa tiba nusu tani kupitia Shirika la Afya Duniani, WHO, pamoja na vifaa vya uzazi 3,500 kupitia Shirika linalohusika na idadi ya watu, UNFPA.