Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwekeza kwa njia endelevu ni jambo la busara katika biashara- Ban

Katibu Mkuu Ban Ki-moon.Picha ya UM/NICA

Kuwekeza kwa njia endelevu ni jambo la busara katika biashara- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kuwa kuna busara kubwa katika kuwekeza kwa njia endelevu, akiongeza kuwa uwekezaji katika sekta ya umma na sekta binafsi umechangia mno katika hatua za kufikia malengo ya maendeleo ya milenia.

Ban amesema hayo katika ujumbe wake wa video kwa kikao cha ufunguzi cha Jukwaa la Uwekezaji Duniani, ambalo limefunguliwa leo mjini Geneva. Amesema uwekezaji utakuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuleta maendeleo endelevu.

Akigusia Ripoti ya Uwekezaji Ulimwenguni mwaka 2014, ambayo ilitolewa na Kamati ya  biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD , Ban amesema ripoti hiyo inadokeza jinsi wadau wote wanavyoweza kushirikiana kuziba mapengo yaliyosalia katika kufikia malengo ya maendeleo ya milenia, akisifu mpango wa UNCTAD wa hatua za uwekezaji wa kibinafsi katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Katibu Mkuu amesema kuwa mbinu zinazotumiwa na sekta ya kibinafsi zinaweza kusaidia katika uvumbuzi.