Mkuu wa MONUSCO atoa wito makundi ya wawindaji haramu Garamba yakomeshwe
Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, MONUSCO, Martin Kobler, ametoa wito kwa watendaji wa kitaifa na kimataifa kujiunga na juhudi za kuhifadhi rasilimali kubwa na utajiri wa asili na viumbehai wa hifadhi ya kitaifa ya Garamba, ilioko kaskazini-mashariki mwa DRC.
Bwana Kobler amesema hayo wakati wa ziara yake kwa hifadhi ya Garamba pamoja, akiwa ameandamana na Naibu Balozi wa Marekani nchini DRC, Balozi wa Morocco na baadhi ya maafisa wa Uongozi wa Ujumbe wa MONUSCO, Kobler amesema, makundi yaliyojihami mashariki mwa DRC kwa kiasi kikubwa hufadhiliwa na mapato yatokanayo na biashara haramu na uuzaji wa rasilimali, lakini amesema juhudi dhidi ya makundi hayo ni lazima ziangazie chanzo cha vita pia.
Katika miaka ya hivi karibuni, kuongezeka kwa ujangili kumeangamiza sana idadi ya wanyamapori katika hifadhi ya Garamba.
Kulingana na usimamizi wa hifadhi hiyo, licha ya juhudi dhidi ya ujangili, zaidi ya tembo 60 wameuawa tangu Aprili 2014, wahalifu wakuu wakiwa ni makundi yenye silaha muhimu zaidi ikiwa ni lile la kundi la Lord’s Resistance Army, LRA .
Mkuu huyo wa MONUSCO aliwapongeza walinzi wa hifadhi ya Garamba, Taasisi ya Kongo ya hifadhi ya asilia, na wadau mbali mbali kwa jitihada zao za kulinda hifadhi ya kitaifa ya Garamba, lakini pia ameelezea haja ya juhudi za pamoja za kuondokana na tishio la makundi ya waasi na shughuli zao za kinyume cha sheria.