Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziarani Libya, Ban atolea wito makubaliano ya amani

mji wa Misrata, nchini Libya. Picha ya UNHCR/Helen Caux

Ziarani Libya, Ban atolea wito makubaliano ya amani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amewasili Libya jumamosi tarehe 11 Oktoba akizisihi pande zote kufikia makubaliano ya amani ili kurejesha hali ya utulivu nchini humo.

Amesema lengo la mapinduzi ilikuwa ni kupata uhuru na maisha bora, lakini mapigano yasipositishwa, maisha bora yatabaki tu ndoto.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Ban ametaka bunge la Libya liwakilishe raia wote na mamlaka za serikali ziwe na nguvu zaidi, akisema utawala bora na mazungumzo ya kisiasa ndivyo vitakomesha ugaidi.

Katibu Mkuu amekutana na baadhi ya wabunge wa Libya pamoja na mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Bernandino Leon.

Tangu kupinduliwa kwa serikali ya Gaddafi, maelfu ya raia wa Libya wameuawa au kulazimika kukimbia makwao. Kwa kipindi cha wiki tatu zilizopita, zaidi ya watu 100,000 wamekimbia makwao kutokana na mapigano katika mji mkuu wa Tripoli.