Mapigano Kobane, De Mistura atoa ombi kwa Uturuki

10 Oktoba 2014

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura, ametoa ombi kwa serikali ya Uturuki iruhusu wananchi wanaotaka kujitolea kupigana ili kutetea eneo la Kobane ambalo sasa linatishiwa usalama wake na wapiganaji wa ISIS.

De Mistura amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi.

(Sauti ya De Mistura)

“Tunaiomba serikali ya Uturuki iruhusu watu wanaotaka kujitolea kuingia ndani ya mji wa Kobane, pamoja na vifaa vyao, ili washiriki kwenye operesheni ya ulinzi.”

Mjumbe huyo amesema Umoja wa Mataifa hautaki kushuhudia tena mauaji kama yaliyotokea Srebrenica, nchini Bosnia mwaka 2005.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, zaidi ya wakurdi 172,000 wamekimbilia Uturuki kutokana na mapigano katika maeneo ya Kobane, wengine wakitafuta hifadhi katika maeneo ya kikurdi ya Iraq.

UNHCR imekariri ripoti moja inayonukuu wakimbizi wakisema kuwa wamepata mateso ya aina mbalimbali, wengine wakisema vichwa vya wafungwa waliouawa na ISIL vimening’inizwa kwenye baadhi ya kuta huko Kobane, ili kutisha watu wengine.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter