Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama yalaani vikali mashambuzi dhidi ya MINUSCA.

UN Photo/Paulo Filgueiras
Picha:

Baraza la Usalama yalaani vikali mashambuzi dhidi ya MINUSCA.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali shambulizi dhidi ya msafara wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA, uliotokea Alhamisi ambapo mwanajeshi mmoja wa kulinda amani kutoka Pakistan aliuawa huku wengine kutoka Pakistan na Bangladesh wakijeruhiwa vibaya.

Katika taarifa, wanachama wa Baraza la Usalama wametuma rambirambi zao na masikitiko kwa familia ya mlinda amani aliyeuawa, halikadhalika serikali za Pakistan na Bangladesh na mamlaka ya mpito nchini CAR na ujumbe wa MINUSCA.

Wanachama wa Baraza la Usalama wameiomba mamlaka ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kulaani vikali shambulizi dhidi ya MINUSCA na kuanzisha uchunguzi wa haraka ikisaidiana ujumbe huo na kuwachukulia hatua za kisheria waliotekeleza kitendo hicho.

Pamoja na kuelezea wasiwasi wao kuhusu ongezeko la vurugu katika siku za hivi karibuni mjini Bangui na kutaka zisitishwe, wanachama hao wamesisitiza kuwa waliotekeleza kitendo hicho lazima wawajibishwe.