Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushindi wa Tuzo la Nobel ni ujumbe muhimu: Zeid Ra'ad Al-Hussein

UN Photos/ Paulo Filgueiras
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein@

Ushindi wa Tuzo la Nobel ni ujumbe muhimu: Zeid Ra'ad Al-Hussein

Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu, Zeid Ra'ad Al-Hussein amesema ushindi wa tuzo ya Amani ya Nobel kwa watetezi wawili wa haki za watoto ni ujumbe muhimu wa kuunga mkono na kutambua watu ambao wanahaha duniani kote bila kuchoka kutetea haki za watoto.

Washindi hao wa mwaka huu ni Malala Yousafzai wa Pakistani na Kailash Satyarthi wa India.

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu imemkariri Zeid Ra'ad Al-Hussein akisema Malala na Kailash wameonyesha ujasiri mkubwa licha ya kukabiliwa na changemoto nyingi.

Mathalani amesema Malala ambaye yeye mwenyewe ni mtoto amekabiliana na makundi yaliyojihami katika harakati zake za haki ya elimu kwa wasichana na wavulana.

Kwa upande wake, Kailash amekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya kutumikishwa kwa watoto ambayo ni sawa na kuwashirikisha watoto kibishiara.

Aidha, Zeid Ra'ad Al-Hussein, amesema anatumai tuzo hiyo kwa watetezi hao wa kipekee itatumika kuimarisha utashi wa kisiasa wa mataifa na kupatia msukumo juhudi za taasisi na ya watu binafsi duniani za kuzingatia haki za watoto ambao ni rasilimali iliyo na thamani zaidi.