Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awapongeza washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Malala Yousafzai na Kailash Satyarthi

UN Photo/NICA
Washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka 2014, Malala Yousafzai na Kailash Satyarthi. Picha:

Ban awapongeza washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Malala Yousafzai na Kailash Satyarthi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amewapongeza Malala Yousafzai na Kailash Satyarthi, ambao ndio washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka, akiwataja kuwa miongoni mwa mabingwa wakubwa zaidi  wa kutetea watoto.

Akimtaja kama binti wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban amemsifu Malala kama mtetezi wa amani jasiri na mnyenyekevu, ambaye kupitia hatua yake ya kwenda shule, aliweza kuwa mwalimu wa ulimwengu mzima. Katibu Mkuu amesema kupitia ujasiri wake na kupiga moyo konde, Malala ameonyesha kile ambacho magaidi wanaogopa zaidi: mtoto wa kike akiwa na kitabu.

Aidha, Katibu Mkuu amemsifu Bwana Kailash Satyarthi kama mtu aliyekuwa mstari wa mbele kwenye msukumo wa kimataifa wa haki, elimu ya kimataifa na maisha bora kwa mamilioni ya watoto walionaswa katika ajira za watoto.