Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakutana na makamanda wa vikosi vya kulinda amani

UN photo / Catianne Tijerina
( picha ya

Baraza la Usalama lakutana na makamanda wa vikosi vya kulinda amani

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limefanya kikao kuhusu operesheni za ulinzi wa amani katika Umoja wa Mataifa, ambapo limehutubiwa na makamanda wa vikosi mbali mbali vya kulinda amani, akiwemo kamanda wa kwanza wa kike. Joshua Mmali amekifuatilia kikao cha leo.

(Taarifa ya Joshua)

Akiwatambulisha makamanda hao mbele ya Baraza la Usalama, Mshauri wa Kijeshi wa Idara ya Ulinzi wa Amani katika Umoja wa Mataifa, Luteni Jenerali Maqsood Ahmed, amesema makamanda hao wanaongoza zaidi ya wanajeshi elfu 90, na aghalabu katika mazingira magumu mno.

(Sauti ya Maqsood)

Mali ni mfano wa mahali ambapo tumepoteza wanajeshi wengi zaidi mwaka huu. Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan, Sudan Kusini na Darfur, Golan na MONUSCO ni kwingineko kwenye changamoto. Makamanda hawa wanafanya kazi katika mataifa yanayosambaratika au yaliyosambaratika, ambapo kusema kweli hakuna amani ya kulinda. Ebola ni aina nyingine ya ugumu huo.”

Makamanda hao wamehutubia kuhusu ulinzi wa raia, matarajio kutoka kwa vikosi vya kijeshi katika mazingira yaliyobadilika kiusalama, pamoja na utekelezaji wa majukumu ya ulinzi wa amani katika mazingira yaliyobadilika kisiasa na kijeshi. Akizungumza kuhusu ulinzi wa raia, Luteni Jenerali Carlos Alberto dos Santos Cruz ambaye ni kamanda wa kikosi cha kulinda amani Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, MONUSCO, ameelezea njia bora ya kuwalinda raia.

(Sauti ya Santos Cruz)

“Kutambua na kuchukua hatua dhidi ya tishio linaloletwa na makundi yenye silaha ambayo ndiyo yanayotekeleza ukatili wa moja kwa moja kama vile ubakaji, uporaji, mauaji na uhalifu mwingine, kutasaidia zaidi kuliko kusubiri hadi matukio haya yafanyike.”