Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlioahidi misaada dhidi ya Ebola timizeni: Ban atoa rai

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.Picha@UM

Mlioahidi misaada dhidi ya Ebola timizeni: Ban atoa rai

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amerejelea wito wake hali ya ugonjwa wa Ebola itakuwa mbaya kabla ya kudhibitiwa na hivyo kutaka nchi zilizotoa ahadi kukabili mlipuko huo kutekeleza ahadi zao. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Ban amesema hayo katika kikao cha ngazi ya juu kilichoandaliwa na Benki ya dunia na shirika la fedha duniani, IMF mjini Washington DC, wakati huu Ebola inazidi kuwa tishio duniani.

Katibu Mkuu amesema msaada unatakiwa kuongezeka angalau mara 20 zaidi akitaja vinavyotakiwa kuwa ni maabara zinazoweza kuhamishwa kutoka eneo moja hadi lingine, helikopta, vifaa vya kujikinga na wataalamu wenye ujuzi.

Amesema ni lazima kushirikiana kutoka huduma bora zaidi kwa kila mgonjwa, kwani hali itakuwa mbaya zaidi kabla ya kuimarika akikumbusha kuwa kiwango cha ubaya kinategemea kasi ya hatua zitakazochukuliwa na jamii ya kimataifa.

Kikao hicho kilihutubiwa pia na viongozi wa Guinea, Sierra Leone na Liberia ambapo Rais Alpha Condé wa Guinea ametoa rai ya kuwepo kwa uratibu madhubuti wa harakati dhidi ya ugonjwa huo akitolea mfano kuwa fedha zinatolewa lakini kama hakuna umakini kuna uwezekano wa kuibuka kwa rushwa na matumizi mabaya.