Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makadirio ya IMF yaonyesha matumaini ya ukuaji wa uchumi Afrika

nembo ya Shirika la fedha Duniani, IMF

Makadirio ya IMF yaonyesha matumaini ya ukuaji wa uchumi Afrika

Shirika la Fedha Duniani, IMF. Limekadiria kuwa ukuaji wa kiuchumi duniani utasalia kwa kiwango cha asilimia 3.3 mwaka huu, na kupanda hadi asilimia 3.8 mwaka 2015.

Kiwango hicho ni hafifu kidogo, kikilinganishwa na makadirio ya awali, lakini hali inatofautiana kote duniani, kwa mujibu wa Mtaalamu Mkuu wa masuala ya Uchumi katika IMF, Olivier Blanchard:

Sauti ya Olivier Blanchard  1

“Uchumi unakua tena, lakini ni hafifu, na hakuna usawa.”

IMF inakadiria kuwa baadhi ya chumi zilizokuwa kama vile za Marekani, huenda zitaendelea kukua, na hali hii itakuwa na faida kwa nchi jirani katika ukanda na zile zinazofanya biashara nazo, lakini nchi nyingi duniani bado zinaishi na athari za mdororo wa uchumi duniani wa mwaka 2008.

Sauti ya Olivier Blanchard 2

"Kwa hiyo, katika chumi zilizoendelea, sera ni lazima zikabiliane na madhara ya mdororo huo, na kwa mtazamo wa mbele, zikabiliane na suala la ukuaji wa mwendo wa pole.”

Kwa masoko yanayoibuka, ukuaji umetabiriwa kushuka kwa takriban asilimia 4.4 mwaka 2014, hali ambayo inaelezwa kusababishwa na ununuzi mdogo wa biashara kitaifa na kuongezeka kwa migogoro ya kisiasa, ukiwemo ule kati ya Urusi na Ukraine.

Ingawa makadirio kwa nchi nyingi ni hafifu kuliko ilivyotarajiwa, nchi za kipato cha chini, hususan Kusini mwa Jangwa la Sahara, zimetabiriwa kuendelea kufurahia viwango vya juu vya ukuaji, kwa mujibu wa Rupa Duttagupta, afisa wa IMF.

Sauti ya Rupa Duttagupta

“Mtazamo wetu ni kwamba ukanda huo utaendelea kukua kwa kasi thabiti ya asilimia 5.1, ambayo itaendelea kwa muda, na hata kuongezeka.”

Duttagupta amesema pia kuwa changamoto zinazozikabili nchi za Afrika Magharibi, ambazo zimeathiriwa na baa la Ebola, akitaja ahadi ya IMF hivi karibuni ya dola milioni 130 kusaidia kupunguza mzigo wa kiuchumi wa baa hilo. IMF pia imezishauri nchi ziendelee kuwekeza katika miundo mbinu, hata kama zinakabiliana na mzigo wa kiuchumi.