Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bajeti ya UNMEER yaidhinishwa, ni takribani dola Milioni 50.

Moja ya huduma zinazohitajika ni pamoja na vifaa na maji yenye dawa za kutakatisha mikono kuepusha vijidudu kama ilivyo ndoo hii katika moja ya kliniki za Ebola, Monrovia, Liberia. (Picha:UNMIL/Staton Winter)

Bajeti ya UNMEER yaidhinishwa, ni takribani dola Milioni 50.

Kamati ya Tano ya masuala ya fedha ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imeidhinisha takribani dola Milioni 50 kwa ajili ya ujumbe wa dharura wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia Ebola, UNMEER na ofisi ya mjumbe maalum kuhusu ugonjwa huo kwa kipindi cha mwaka huu.

Uamuzi huo umetangazwa Jumanne wakati wa kikao cha kamati hiyo ambapo Rais wa Baraza Kuu Sam Kutesa amesema ni kiashiria thabiti cha kamati hiyo katika kushughulikia masuala ya dharura duniani.

Pendekezo la bajeti hiyo liliwasilishwa Ijumaa mbele ya kamati hiyo wakati huu ambapo baadhi ya watendaji wa UNMEER wameshapelekwa kwenye makao makuu ya ofisi hiyo mjini Accra, Ghana.

Kutesa amesema changamoto sasa ni kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo na kutoa usaidizi unaotakiwa kwenye nchi zinazohusika.

Hadi sasa watu zaidi ya 6500 wameugua ugonjwa huo kati yao zaidi ya 3,300 wakifariki dunia huko Guinea, Liberia na Sierra Leone.