Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya makazi duniani tusikilize sauti ya wanaoishi kwenye makazi duni: UN- Habitat

UN-Habitat)
Julius Mwelu
Mara nyingi makazi duni yanapoboreshwa, wanufaika ni matajiri. Pichni ni moja ya makazi duni nchini Haiti,

Siku ya makazi duniani tusikilize sauti ya wanaoishi kwenye makazi duni: UN- Habitat

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na makazi, UN-Habitat limesema watu Bilioni Moja duniani wanaishi kwenye makazi duni, wakikosa huduma nyingi za msingi zikiwemo maji na usafi, barabara na usafiri.

Shirika hilo limesema pamoja na kuishi kwenye mazingira hayo, watu hao pia wanaathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi wakiwa hatarini kukumbwa na mmomonyoko wa ardhi au mafuriko.

Ni kutokana na hali hiyo, ujumbe wa mwaka huu wa siku ya makazi duniani leo tarehe Sita Oktoba unaangazia hatma ya wakazi hao ambapo  Mkurugenzi Mkuu wa UN-Habitat, Dkt. Joan Clos, anasema maisha ya watu milioni 200 yameimarishwa tangu mwaka 2000, lakini bado juhudi zahitajika.

Kwa mujibu ya UN-Habitat idadi ya watu wanaoishi kwenye makazi duni inaendelea kuongezeka.

Dkt Clos amesema ni vyema  kusikiliza sauti za wakazi hao ambao wanaomba kupatiwa haki zao za huduma za msingi.

Aidha amesema suluhu endelevu kwa makazi duniani ni kuboresha mpango kazi za ujenzi wa miji akitaka  serikali ziangazie jinsi ya kuhakikisha kuwepo kwa nyumba za bei nafuu, barabara, mifereji ya majitaka, umeme na maji wakati wa ujenzi wa  mitaa mipya kwenye miji.

Mkuu huyo wa UN-Habitat  amesema kushughulikia matatizo ya maeneo ya makazi duni kutainua  maisha ya wakazi wao, na kuleta matokeo makubwa kiuchumi na kijamii.