Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi 18 wa Syria wapata hifadhi Ufaransa:IOM

Wakimbizi wanawake wa Syria.Picha ya UNHCR/N. Daoud

Wakimbizi 18 wa Syria wapata hifadhi Ufaransa:IOM

Shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM limesema wakimbizi 18 wa Syria wamefanikiwa kupata hifadhi nchini Ufaransa kupitia mpango wa pamoja wa kibinadamu baina ya serikali ya Ufaransa, IOM na shirika la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR.

Mkuu wa IOM nchini Ufaransa Sara Abbas amesema mpango huo wa kibinadamu uliotangazwa na Rais wa Ufaransa unalenga kuwapatia hifadhi jumla ya wakimbizi 500 wa Syria mwaka huu pekee,.

Tangu mwezi Januari mwaka huu wakimbizi wa Syria wamekuwa wakiwasili nchini Ufaransa wakitokea Lebanon, Jordan na Misri.

Bi. Abbas amesema kupitia mpango huo, ofisi za IOM ufaransa na kule wanakotoka wakimbizi hao wanashirikiana kwenye mchakato wa kuwasaidia wakimbizi hao ambao wengine wao wanakuwa kwenye hali mbaya.

Usaidizi ni pamoja na kuandaa nyaraka, uchunguzi wa tiba, kuwasindikiza wale wanaohitaji msaada na hata kufanya uratibu na mamlaka za Ufaransa kwenye masuala ya elimu, ajira na hata malazi.

Tangu mwaka 2008, ofisi ya IOM nchini Ufaransa imesaidia kuwapatia hifadhi zaidi ya wakimbizi 2,000 kutoka mataifa 30 tofauti.