WFP yaendeleza msaada wake kwa wahanga wa Ebola

3 Oktoba 2014

Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola, UNMEER Anthony Banbury amewasili nchini Sierra Leone kutathmini hali halisi wakati huu ambapo idadi ya vifo imefikia 3,338.

Banbury anafanya ziara hiyo wakati Shirika la Chakula Duniani WFP likitangaza kufikisha chakula kwa zaidi ya watu 430,000 walioathirika na mlipuko wa Ebola likieleza pia kusambaza misaada ya aina nyingine.

Mkurugenzi wa WFP Kanda ya Afrika Magharibi, Denise Brown, amesema WFP haipeleki tu chakula bali pia vifaa, usafiri wa ndege, boti na helikopta, ikishughulikia pia kujenga vituo vinne vya afya nchini Liberia.

Akizungumza na Idhaa hii, Msemaji wa WFP, Elizabeth Byrs amesema msaada wa chakula unalenga wagonjwa, waliopona na Ebola, na familia za wagonjwa, mahitaji ya chakula yakitathminiwa kupitia mfumo mpya wa simu za mkononi.

“Lengo la operesheni hii ni kuzuia maambukizi ya virusi, tunaona kwamba masoko hayafanyi kazi tena. Watu hawana pesa kununua vyakula vyao. Na wakilazimika kutembea kilomita kadhaa ili kununua chakula chao kwa ajili ya mahitaji yao, wakiweza kutembea, wako hatarini ya kuambukizwa.”

Halikadhalika amesema WFP ina wasiwasi sana juu ya athari za kiuchumi za mlipuko huo wa Ebola kwa kuwa watu wameacha kulima mashamba yao kwa muda.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter