Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua madhubuti zahitajika haraka kufikia malengo ya Bayo-anuai 2020- ripoti

Picha ya Maktaba: UM

Hatua madhubuti zahitajika haraka kufikia malengo ya Bayo-anuai 2020- ripoti

Hatua mathubuti na bunifu zinahitajika haraka iwapo serikali zinataka kutimiza mpango wa mkakati uliokubaliwa kimataifa na malengo ya Aichi ifikapo mwaka 2020, imesema ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya bayo-anuai duniani.

Ripoti hiyo ambayo imezinduliwa leo mwaka mmoja kabla ya kufikia nusu ya safari ya mpango wa mkakati kuhusu Bayo-anuai wa 2011-2020 na Mwongo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bayo anuai, unaonyesha kuwa kuna ufanisi katika sehemu fulani za kutimiza malengo hayo. Licha ya hatua hizo, ripoti imesema kuwa hatua zaidi zinahitajika ili kuuendeleza mpango huo mahsusi wa 2011-2020 kwenye mkondo sahihi.

Mpango wa mkakati wa 2011-2020  kuhusu Bayo-anuai na Malengo ya Aichi kuhusu Bayo-anuai, uliafikiwa na jamii ya kimataifa mnamo mwaka 2010 mjini Nagoya, Japan, na ukaridhiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na pia kwenye mkutano wa Rio +20 kuhusu Malengo ya Maendeleo ya Milenia, SDGs mnamo mwaka 2012.  Kuyafikia malengo hayo kunatarajiwa kuchangia pakubwa katika masuala ya kipaumbele ya ajenda ya maendeleo baada ya 2015, yakiwa ni pamoja na kupunguza njaa na umaskini, kuboresha afya ya wanadamu, nishati endelevu, chakula na maji safi.

Ripoti hiyo imesema kufikia malengo haya ya pamoja kunahitaji mabadiliko katika jamii, yakiwemo matumizi bora ya ardhi, maji, nishati na kufikiria tena kuhusu jinsi chakula kinavyozalishwa na kutumiwa.