Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakaribisha mkutano wa kisiasa uliofanyika Libya

UN Photo/Paulo Filgueiras
Mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu Mashariki ya Kati.

Baraza la Usalama lakaribisha mkutano wa kisiasa uliofanyika Libya

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamekaribisha mkutano baina ya wawakilishi wa bunge ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa na kufanyika mjini Ghedames mnamo tarehe 29 Septemba kama hatua muhimu ya kupatia suluhu la amani mkwamo wa kisiasa uliopo nchini Libya.

Wanachama wa Baraza la Usalama wameelezea uungaji mkono wao wa dhati kwa juhudi za kushughulikia tofauti zilizopo baina ya pande husika kupitia mazungumzo jumuishi ya amani, katika utaratibu wa harakati za kisiasa.

Wanachama hao wa Baraza la Usalama wametoa wito kwa pande zote kupinga ghasia na kujikita katika harakati za kisiasa. Wamekumbusha pia kuhusu azimio namba 2174 (2014), wakisema wa tayari kutumia vikwazo vya kulenga, vikiwemo vya mali na usafiri, dhidi ya watu na makundi yaliyotishia amani na utulivu Libya au kuvuruga mpito wa kisiasa.