Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zichukuliwe kuepusha Lampedusa nyingine: UNHCR

Boti ikiwasili katika kisiwa cha Lampedusa (Picha ya maktaba/UNHCR)

Hatua zichukuliwe kuepusha Lampedusa nyingine: UNHCR

Kuelekea mwaka mmoja tangu kutokea kwa janga la kuzama kwa boti iliyokuwa na wahamiaji huko Lampedusa, kwenye bahari ya Mediteranian, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR imetaka hatua zaidi zichukuliwe kuepusha tukio lingine kama hilo.

Katika taarifa yake, UNHCR imesema takwimu za robo ya tatu ya mwaka huu pekee zinaonyesha ongezeko la idadi ya watu wanaofariki dunia wakati wakisafiri kwa njia zisizo halali kwenda Ulaya kusaka maisha bora.

Kati ya Julai na Septemba watu 90,000 walivuka kuingia Ulaya ambapo kati yao hao 2,200 walifariki dunia ikilinganishwa na 75,000 waliovuka Januari hadi Juni na kati yao 800 tu kufariki dunia.

Kwa mantiki hiyo shirika hilo linazisihi nchi za Ulaya kutenga rasilimali zaidi za uokozi kwenye bahari hiyo ya Mediteranian huku ikitaka ziimarishe fursa mbadala za kuwezesha watu kuingia barani huko kihalali badala ya kutumia njia hatari.

Ajali ya kuzama boti kwenye kisiwa cha Lampedusa pwani ya Italia tarehe Tatu Oktoba mwaka jana ilisababisha vifo vya wahamiaji zaidi ya 300.