Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baa la nzige Madagascar lasitishwa, lakini bado kuna hatari ya kurejea

Baa la nzige Madagascar lasitishwa, lakini bado kuna hatari ya kurejea

Nzige waliokuwa wameenea kote nchini Madgascar na kutishia mimea inayotegemewa kwa chakula na malisho ya mifugo sasa wamekomeshwa, kwa mujibu wa Shirika la Kilimo na Chakula, FAO.

Nzige hao walioanza kuvamia mwezi Aprili mwaka 2012 waliharibu mimea na malisho wakitokea kusini mwa nchi na kuelekea kaskazini, na kufikia Aprili mwaka huu, walikuwa wameenea hadi eneo la kaskazini magharibi mwa nchi kunakozalishwa mpunga kwa kiasi kikubwa zaidi, na hivyo kutishia vipato vya watu milioni 13.

Uwezekano wa uharibifu zaidi ulizuiwa na kampeni ya kwanza ya kuzuia nzige, ambayo ni sehemu ya mpango wa pamoja wa miaka mitatu unaotekelezwa na FAO na serikali ya Madagascar.

Hata hivyo, FAO inasema kuwa inahitaji ufadhili zaidi ili kuendelea kuendelea na mpango huo wa kuwadhibiti nzige, ikiongeza kuwa hali huenda ikazorota wakati msimu wa mvua ukianza mwezi Oktoba, kwani hali ya joto wakati huu ni mazingira bora kwa  nzige kuongezeka idadi yao.

Annie Monard ambaye ni Mratibu wa mpango wa FAO wa kukabiliana na dharura ya tatizo hilo amesema kuwa dola milioni 14.7 zinahitajika haraka kwa kufanya tathmini ya angani, operesheni za kudhibiti, vifaa kazi, dawa za kuua nzige na pia kuajiri wahudumu muhimu wa kuetekeleza kampeni ya pili na tatu.

"Tumefanikiwa katika kulisitisha baa lakini kama hapatakuwa na kampeni ya pili na ya tatu, baa linaweza kuibuka tena wakati wowote. Lakini nzige wako tayari kuongezeka tena kwa haraka mvua zikianza na kuna haja ya kuwa tayari kabisa wakati huo na kuwa na uwezo wa kupunguza na kukomesha uanguzi mpya wakati wa msimu wa pili wa mvua, la sivyo, baa lingine litaanza tena na kuleta madhara ya usalama wa chakula na matatizo kwa wanadamu. "

Awamu ya kwanza ya mpango wa kudhibiti nzige Madagascar uligharimu dola milioni 28.