Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon alaani mashambulizi ya Homs

Adnan, mtoto wa miaka mitano aliyejehuriwa wakati wa mashambulizi nchini Syria. Picha ya UNICEF/Marta Ramoneda

Ban Ki-moon alaani mashambulizi ya Homs

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali mashambulizi ya mabomu yaliyotokea tarehe mosi Oktoba katika mji wa Homs, nchini Syria na kuua watu 39, wakiwemo wanafunzi 30 wenye umri kati ya miaka sita na tisa, kwa mujibu wa ripoti za awali zilizotolewa.

Amesema tukio hilo ni upotovu uliokithiri, akirudia wito wake kwa pande zote za mapigano hayo kusitisha mashambulizi dhidi ya raia.

Katibu Mkuu amepeleka rambirambi zake kwa familia za wahanga akiwatakia nafuu waliojehuriwa.

Kwa upande wake mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, nchini Syria Hanaa Singer, amesema juhudi mpya zinahitajika ili kusitisha msururu huu wa ukatili usiokuwa na maana, akikumbusha pande zote kwamba wanapaswa kulinda raia wa kawaida na kuheshimu sehemu za shule kama sehemu za hifadhi kwa haki za watoto.