Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon: Siku ya Kupinga Ukatili Duniani, tukumbuke ujumbe wa Mahatma Gandhi

Bastola iliyopo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa ni ishara ya msimamo wa kupinga ukatili na vurugu. Picha ya UN Michos Tzovara.

Ban Ki-moon: Siku ya Kupinga Ukatili Duniani, tukumbuke ujumbe wa Mahatma Gandhi

Tarehe 2, mwezi Oktoba ikiwa ni siku ya kupinga Vurugu na Ukatili Duniani, Umoja wa Mataifa unaadhimisha pia siku ya kuzaliwa kwa Mahatma Gandhi, Shujaa wa uhuru wa India aliyepigania ukombozi wa nchi yake bila kutumia vurugu, akiwa maarufu kwa kusema:

“ Niko tayari kufa kwa ajili ya kesi nyingi, lakini hakuna kesi moja ambayo niko tayari kuua kwa ajili yake."

Katika ujumbe wake kwa siku hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema maadili ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binadamu ulioidhinishwa mwaka 1948 yametokana na maoni ya Mahatma Gandhi kwamba maandamano yenye amani yanaweza kuleta matokeo zaidi ya mapigano.

Bwana Ban ameongeza, wakati huu wa mapigano na uharibifu wa sehemu maarufu za urithi wa kitamaduni duniani, ni muhimu kuendeleza tabia za kuishi pamoja kwa kuheshimiana na kufurahia tofauti za dunia.

Aidha amesema elimu ndiyo njia sahihi ya kujenga mila ya kupinga ukatili na kujenga amani endelevu, akiwaomba watu wote kujenga mshikamano na kuendeleza uraia wa kimataifa.