Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutesa kuanza kushughulikia marekebisho ya mfumo wa Umoja wa Mataifa

Sam Kutesa wakati wa kufungua rasmi kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Kutesa kuanza kushughulikia marekebisho ya mfumo wa Umoja wa Mataifa

Baada ya mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhitimishwa Jumanne tarehe 30 Septemba, Rais wa Baraza hilo Sam Kutesa amewaambia waandishi wa habari mjini New york kwamba mazungumzo hayo yameonyesha uwezekano wa kuleta mabadiliko duniani kupitia ushirikiano wa kimataifa.

Bwana Kutesa amesema, ajenda ya maendeleo ya baada ya 2015, hatari ya ugaidi kwa usalama na amani ya dunia, na mlipuko wa Ebola yalikuwa masuala yaliyozungumzwa zaidi na viongozi wa dunia wakiwemo marais na wakuu wa serikali 117, akisisitiza umuhimu wa kupata suluhu za matatizo hayo kwa kupitia ushirikiano baada ya uamuzi wa upande mmoja.

Aidha amerudia wito wake wa kupunguza idadi ya mikutano inayofanywa wakati wa mjadala mkuu ili viongozi wasihutubie baraza bila watu kuwasikiliza.

Akijibu swali la mwandishi wa habari, ameeleza kuwa mabadiliko ya mfumo wa Umoja wa Mataifa yamezingatiwa sana na baadhi ya viongozi akisema:

“ Nchi nyingi, kwa kweli kila mtu, anatambua kwamba Umoja wa Mataifa ulioanzishwa miaka 70 iliyopita unahitaji kufanyiwa marekebisho ili kukidhi dunia ya leo. Nadhani tunachohitaji kufanya ni kusonga mbele, huenda hatutaweza kukamilisha hicho mwaka huu, wala hata baada ya miaka mitano. Lakini kazi yangu mwaka huu itakuwa ni kujaribu pande zote zikubali kuandika mradi ambao tutaweza kuanza kuzungumzia. Kwa sababu sasa kila mtu anarudia tu msimamo wake wa zamani”