Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajenda Afrika 2063 ni njia ya kubuni ajenda yetu ya maendeleo baada ya 2015- EAC

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC(Picha:uneca)

Ajenda Afrika 2063 ni njia ya kubuni ajenda yetu ya maendeleo baada ya 2015- EAC

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, Charles Njoroge, amesema leo kuwa Ajenda 2063 iliyowekwa na nchi za Afrika wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Afrika, ni njia ya bara hilo kubuni ajenda yake ya baada ya mwaka 2015.

Akizungumza leo mjini New York wakati mkutano wa ngazi ya juu kuhusu mchango wa jumuiya za kikanda katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani Afrika, Bwana Njoroge amesema ni kweli kuwa bara la Afrika limepiga hatua kwa kiasi fulani katika kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia, akitoa mifano

Kama vile elimu ya msingi kwa wote, usawa wa jinsia katika ngazi tofauti za elimu, kupunguza maambukizi ya HIV miongoni mwa vijana kati ya umri wa miaka 15 na 24, kuongeza upatikanaji wa dawa za HIV na kuongeza ushiki wa wanawake katika mifumo ya uwakilishi. Lakini bado kuna kazi nyingi ya kufanya.”

Amesema kinachopaswa kufanywa sasa ni kubadili ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 kuwa ajenda ya mashirika ya umma, bunge, serikali za mikoa, na kuzichagiza nchi wanachama wa AU kuifanya Ajenda ya Afrika 2063 kuwa ajenda ya maendeleo ya kitaifa, kwa kuchukua hatua mathubuti na kutimiza ahadi.

Tunapofanya hivi, bila shaka tunahitaji uungwaji mkono wa Umoja wa Mataifa na wadau wengine. Kuna haja ya kuungwa mkono mikakati yetu ya kuimarisha taasisi, hususan katika nyanja za kiuchumi na kijamii, na utawala wa kisiasa. Jumuiya za kikanda zinahitaji kuungwa mkono ili kuioanisha mipango yao na Ajenda Afrika 2063.”