Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yajulishwa juu ya kisa cha Ebola Marekani

Picha: WHO/N. Alexander

WHO yajulishwa juu ya kisa cha Ebola Marekani

Shirika la afya ulimwenguni WHO na shirika la afya nchini Marekani PAHO limejulishwa kisa kimoja cha mgonjwa wa homa ya Ebola nchini Marekani katika jimbo la Texas nchini humo.

Taarifa ya WHO inasema mgonjwa huyo mtu mzima hivi karibuni alisafiri kwenda Afrika Magharibi alionekana kuwa na dalili za Ebola tarehe 24 September siku nne baada ya kurejea Marekani na kuwa mtu huyo hakuwa na dalili wakti akiondoka Afrika Magharibi.

Kwa mujibu wa WHO mgonjwa huyo alitafuta tiba mnamo September 26 na kuweka katika wodi maalum iliyotengwa September 28 katika hospitali iiitwayo Texas Health Presbyterian Hospital iliyoko Dallas.

WHO inasema kuwa sampuli zilitumwa kwenye kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa jimboni Atlanta Georgia na maabara ya Texas ambapo ilithibitika kuwa ana virusi vya Ebola.

Hata hivyo taarifa imeeleza kuwa katika hatua ya kuzuia uenezaji wa Ebola nchini Marekani hatua za kuwasaka abiria waliosafiri pamoja na mgonjwa huyo katika ndege hazitachukuliwa kwa kuzingatia ukweli kuwa hakuwa na dalili kabla ya safari kutoka Afrika Magharibi.