Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajenda 2063 inaashiria utashi wa kisiasa kuendeleza Afrika

UN Photo/Paulo Filgueiras
Maged Abdelaziz.

Ajenda 2063 inaashiria utashi wa kisiasa kuendeleza Afrika

Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Afrika, Maged Abdelaziz, amesema kuwa Ajenda 2063 ambayo iliridhiwa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, AU, inaonyesha utashi mpya wa viongozi wa kisiasa barani Afrika wa kufikia ndoto ya pamoja ya bara lenye umoja, maendeleo na amani, vyote hivyo vikichochewa na watu wake wenyewe.

Bwana Abdelaziz amesema hayo wakati wa mkutano wa ngazi ya juu kuhusu mchango wa jumuiya za kikanda katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani Afrika, ambao umefanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, new York.

Amepongeza kauli mbiu ya ajenda hiyo, ambayo inasema kuwa ndoto ya bara la Afrika wanalotaka kuliona watu wake, itatimia tu kupitia mchango muhimu wa jumuiya za kikanda, ambazo ni msingi wa umoja na muungano wa bara zima.

Amesema muungano unaotazamiwa katika Ajenda 2063 hauhusu tu jumuiya za kikanda kujikita katika ushirikiano wa kiuchumi kikanda, bali ni wito wenye nguvu kwa uhusiano baina ya amani, usalama na maendeleo.

Ni hakikisho kuwa miungano na ushirikiano wa kikanda ni njia muhimu za kufikia ukuaji wa kiuchumi jumuishi na endelevu, ambavyo vitasaidia bara Afrika kukabiliana na changamoto zinazolikumba, zikiwemo umaskini, mizozo na vita, uenezaji wa misimamo mikali na magonjwa, kama vile dharura ya umma iliyotokana na mlipuko wa Ebola hivi karibuni.”