Banbury akutana na Rais wa Liberia, wajadili kile kinachohitajika kudhibti Ebola

1 Oktoba 2014

Mkuu wa ujumbe mpya wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia dharura ya ugonjwa wa Ebola (UNMEER) Anthony Banbury amewasili nchini Liberia kwa ziara ya siku mbili ambapo tayari amekuwa na mazungumzo na Rais Ellen Johnson Sirleaf.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Monrovia Bwana Banbury amesema Rais Sirleaf ametoa shukrani zake kwa harakati za Umoja wa Mataifa na wadau za kukabiliana na Ebola nchini mwake na kutaja kile ambacho wangalipenda kuona kinatekelezwa.

(Sauti ya Banbury)

Amepatia kipaumbele suala la kasi, ufanisi na umiliki wa kitaifa wa  harakati dhidi ya ebola na hilo linaendana vyema na vipaumbele vya UNMEER.”

Bwana Banbury akaelezea matarajio ya ujumbe wake baada ya ziara hiyo.

(Sauti ya Banbury)

“Tumejizatiti kuwa na uelewa mzuri zaidi wa mahitaji ya haraka zaidi. Mahitaji ni yapi, pengo liko wapi kwenye hatua dhidi ya Ebola, na tutajaribu kuziba pengo hilo haraka iwezekanavyo.”

Tangu uibuke mwezi Machi mwaka huu, Ebola imekumba watu zaidi ya 6500 huko Liberia, Guinea, na Sierra Leone ambapo kati yao zaidi ya 3000 wamefariki dunia, vifo vingi zaidi vikiripotiwa nchini Liberia.

Nigeria ambayo pia iliripoti kuwa na kisa cha Ebola, tayari imetangaza kuwa hakuna tena Ebola nchini humo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud