Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika imepiga hatua, lakini bado haipo kwenye mkondo wa kutimiza MDGs- Eliasson

UN Photo/Paulo Filgueiras
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson. Picha:

Afrika imepiga hatua, lakini bado haipo kwenye mkondo wa kutimiza MDGs- Eliasson

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, amesema kuwa bara la Afrika limpepiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, akisifu umuhimu wa ushirikiano wa kikanda, lakini licha ya hatua hizo, amesema bara hilo bado halipo kwenye mkondo sahihi wa kufikia malengo ya maendeleo ya milenia. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grece)

Akihutubia kikao cha ngazi ya juu kuhusu mchango wa jumuiya za kiuchumi za kikanda barani Afrika, Bwana Eliasson amesema kuwa jumuiya hizo zimeonyesha utashi wao katika kuendeleza biashara baina ya kanda pamoja na ushirikiano wa kijamii na kiuchumi.

Amesema jumuiya hizo pia zimeonyesha kukuza uwezo wa kukabiliana na vyanzo vya migogoro.

Kuhusu maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Naibu Katibu Mkuu amesema hatua zimepigwa, lakini bado bara Afrika halijatimiza matakwa halali ya watu wake, yakiwemo kupanua nafasi za ajira kwa vijana na kuwawezesha wanawake.

“Tupo hapa leo kuona jinsi tunavyoweza kujitahidi zaidi kupunguza umaskini, kuboresha usalama wa chakula na maji, na kuwawezesha akina mama wengi zaidi na watoto wa Afrika kuishi maisha ya afya. Kuwezesha wanawake ni muhimu mno katika kuchochea maendeleo kwa wote.”

Bwana Eliasson amesema Afrika inaweza kufungua milango ya uwezo na ufanisi iwapo ubaguzi na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana utatokomezwa, na kuwekeza katika mustakhbali wao.