Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za Ulaya zinaweza kuzuia vifo na machungu ya wahamiaji wanaosaka maisha bora

Manusura wa ajali ya boti kisiwa cha Lampedusa (Picha ya maktaba/UNHCR)

Nchi za Ulaya zinaweza kuzuia vifo na machungu ya wahamiaji wanaosaka maisha bora

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu za wahamiaji François Crépeau amesema mikakati ya sasa ya nchi za Ulaya kuzuia wahamiaji kuingia kwenye nchi hizo haitakuwa na mafanikio kwani siyo endelevu.

Ametoa onyo hilo katika barua yake ya wazi iliyowekwa bayana Jumanne akisema kuwa nchi hizo zinapaswa kuweka mifumo mipya ya kihalali ya uhamiaji badala la hatua za sasa za operesheni za misako na hata uokozi wa wahamiaji wanaokumbwa na zahma.

Bwana Crépeau amesema kuweka vizuizi kwenye mipaka ya kimataifa ni jambo lisilowezekana na wahamiaji wataendelea kuwasili kwenye nchi hizo za Ulaya licha ya harakati za kuwazuia ambazo husababisha vifo na machungu kwa wengi wao.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya wahamiaji na wasaka hifadhi 130,000 waliingia bara la Ulaya kwa njia ya majini mwaka huu pekee ikilinganishwa na 80,000 mwaka jana ambapo 800 wamefariki dunia kwenye bahari ya Mediterranean mwaka huu.

Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa ukosefu wa taratibu za wazi na za kisheria za wahamiaji wanaotakiwa katika sekta kama vile kilimo na ujenzi, unafanya wanaofika maeneo hayo wapate ajira hizo kinyume cha sheria na waishi katika mazingira magumu.