Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres atoa wito ufadhili wa kibinadamu ufikiriwe upya idadi ya wakimbizi inapoongezeka

Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, António Guterres.(Picha ya UN/unifeed)

Guterres atoa wito ufadhili wa kibinadamu ufikiriwe upya idadi ya wakimbizi inapoongezeka

Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, António Guterres ameonya leo kuwa mfumo wa kimataifa wa kibinadamu umezidiwa na mizozo mipya Mashariki ya Kati na Barani Afrika, na ile ambayo haijatatuliwa Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Somalia na kwingineko.

Katika taarifa yake kwa mkutano wa kila mwaka wa kamati ya usimamizi ya UNHCR, Bwana Guterres amesema kuwa kuongezeka kwa ufadhili wa kibinadamu duniani ambao umevunja rekodi na kufikia dola bilioni 22 mnamo mwaka 2013, haulingani tena na kasi ya kuongezeka mahitaji ya kibinadamu, na hivyo basi kuhitaji kufikiriwa upya kwa ufadhili wa kibinadamu na maendeleo.

Amesema, pamoja na mzozo unaoendelea Syria, mizozo mipya katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini, Ukraine, na Iraq hivi karibuni zaidi imesababisha mateso makubwa na kuwalazimu watu wengi kuhama makwao. Amesema jamii ya kimataifa imekimbilia kukabiliana na mahitaji ya mizozo hii, lakini kila mzozo mpya unapoibuka, inakaribia ukingo wa uwezo wake kusaidia zaidi, akiongeza kuwa hata sasa usaidizi unaotolewa hautoshi tena.

Guterres amezipongeza nchi zinazoendelea na zile zinazopakana na maeneo ya mizozo kwa kuendelea kuwapa hifadhi na ulinzi wakimbizi 9 kati ya kila wakimbizi 10 duniani.