Eritrea yataka mabadiliko ya mfumo wa Umoja wa Mataifa

30 Septemba 2014

Leo ikiwa siku ya mwisho ya mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Waziri wa mambo ya nje wa Eritrea, Osman Saleh, ametoa wito kwa mabadiliko katika mfumo wa Umoja wa Mataifa.

Amesema dunia imebadilika sana tangu kuundwa kwa Umoja wa Mataifa miaka sabini iliyopita lakini mfumo wake bado haujabadilika, na Umoja huo umeshindwa kupambana na matatizo makubwa yanayokumba dunia ya leo, yakiwemo vita, ugaidi, ukiukaji wa haki za binadamu au umaskini, akiomba Umoja wa Mataifa ujengwe upya, akisema:

(Suti ya Saleh)

“ Ili kurejesha uhusiano na uaminifu kwenye Umoja wa Mataifa, ili uwe ni mfumo unaowakilisha kwa dhati mataifa na raia wote, mfumo ambao mataifa yote, yawe makubwa au madogo, yataheshimu hati yake na sheria ya kimataifa, ni lazima tuunde upya, yaani tujenge upya Umoja wa Mataifa na uwe na demokrasia zaidi”.

Hata hivyo amesema, ni vigumu kutarajia mabadiliko hayo kwa sababu ya ushawishi wa mataifa makubwa yenye madaraka, akiongeza kwamba Eritrea imeathirika sana na ushawishi, kwanzia vita vya ukombozi hadi sasa.

Halikadhalika Bwana Osman ameomba Umoja wa Mataifa kusimamisha vikwazo vilivyowekwa dhidhi ya Eritrea, ili raia wake waweze kujenga taifa lao na kujiendeleza kiuchumi.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter