Baada ya Ebola kupora familia zao sasa yatima wabaki na machungu

30 Septemba 2014

Janga la Ebola lililolipuka huko Afrika Magharibi limekuwa na madhara kwa watoto takribani 3,700 huko Guinea, Liberia na Sierra Leone ambao wamepoteza wazazi wao wote au mmoja, hiyo ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

Shirika hilo limesema idadi kubwa ya watoto hao kwa sasa wanakumbwa na unyanyapaa kutoka kwa familia zao au jamii kwa hofu kuwa wataambukiza ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa UNICEF, hofu na unyanyapaa uliozingira ugonjwa huo sasa vinatishia kumomonyoa familia na hata kuathiri mtangamano wa kijamii kwenye nchi hizo.

Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Magharibi na kati mwa Afrika Manuel Fontaine anasema kwa sasa shirika hilo linaangalia mbinu za kitamaduni na nyinginezo mpya za kuwapatia watoto hao usaidizi ikiwemo wa kisaikolojia kama vile mafunzo kwa waliopona Ebola ili watoe msaada kwa awtoto hao walio kwenye vituo vilivyo chini ya karantini.

(Sauti ya Manuel)

“Idadi ya watoto wanaoachwa pekee yao nyumbani kwa sababu ya Ebola inaongezeka. Kawaida wanapatiwa mlo na jirani, lakini hawajaliwi zaidi ya hayo. Kwa upande mwingine, bahati ni kwamba Liberia na Sierra Leone, kutokana na vita, zimeendeleza mifumo yao ya kisheria ya kulinda watoto. Lakini nadhani changamoto kubwa ni unyanyapaa na shida ya kupata fursa kwa ajili ya watoto hawa.”

Kwa mujbu wa shirika la afya duniani, WHO asilimia 15 ya waliokufa kutokana na Ebola huko Guinea Liberia na Sierra eone ni watoto walio na umri wa chini ya miaka 15.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter