Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Botswana inatiwa hofu na mwenendo wa mizozo ya kikatili duniani- Waziri Skelemani

UN Photo/Amanda Voisard
Waziri wa Mambo ya Nje wa Bostwana, Phandu Skelemani.

Botswana inatiwa hofu na mwenendo wa mizozo ya kikatili duniani- Waziri Skelemani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Bostwana, Phandu Skelemani, ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa nchi yake inatiwa hofu na mwenendo uliopo sasa wa kuongezeka mizozo ya kikatili na kudidimia kwa usalama na utulivu duniani.

Akizungumza wakati wa Mjadala Mkuu wa kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bwana Skelemani amesema hivi sasa ulimwengu unashuhudia viwango vya mateso ya wanadamu ambavyo havijawahi kushuhudiwa, huku maelfu ya watu wasio na hatia wakipoteza uhai wao, na matatizo ya kibinadamu yakiwa yamefikia viwango vya kuwa janga.

“Barani Afrika, kuibuka mizozo katili mara kwa mara katika maeneo fulani ya bara letu, hususan Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati, inatia shaka mno. Hatujashindwa tu kutimiza wajibu wetu kama mataifa kuwalinda watu kutokana na uhalifu usiowajibishwa, uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, lakini pia tunaunga mkono, bila kukusudia, uangamizaji huu wa vizazi vijavyo.”

Waziri huyo ameelezea pia kusikitishwa kwa taifa lake na baadhi ya nchi wanachama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama kuendelea kuzuia juhudi za wenzao za kupatia suluhu hali za mizozo

“Je, Bwana Rais, ni kwa nini wanachama wa jamii ya kimataifa wenye kuwajibika wapuuze wajibu wao mkubwa, wakiendeleza hali ya mkwamo wakati dunia inateketea na kuangamizwa? Mwezi Mei mwaka huu, Baraza la Usalama lilishindwa kupitisha azimio la kutaka kupelea kesi ya Syria kwa Mahakama ya Uhalifu wa Jinai, ICC. Bila shaka hili lilikuwa kinyume na sheria ya kimataifa ya uhalifu.”