Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi ya ugaidi hayajatushangaza- Waziri wa Mambo ya nje wa Syria

Waziri wa Mambo ya nje wa Syria, Walid Al-Moualem, picha ya UN.

Mashambulizi ya ugaidi hayajatushangaza- Waziri wa Mambo ya nje wa Syria

Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya nje wa Syria, Walid El-Moualem, amesema serikali ya Syria ilianza miaka mitatu na nusu iliyopita kuonya dunia kuhusu hatari za ugaidi unaoendelea nchini humo, akiongeza kwamba kupambana na ugaidi kunapaswa kuwekwa kipaumbele na jamii ya kimataifa, si mizozo ya kisiasa au ya kiuchumi.

Akiongea wakati wa kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Waziri huyu ameomba juhudi za kimataifa zifanyike ili kuzuia mashambulizi ya ISIS yasiathiri maeneo mengine ya dunia.

Amekaribisha azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama tarehe 15, mwezi Agosti, mwaka huu, ili kuweka vikwazo vya usafiri na biashara za silaha kwa wanamgambo wa ISIS, na lile la Septemba, 24, kuhusu ajira ya wapiganaji kutoka nchi za nje, akisema anasikitika kuona kwamba bado mabadiliko hayajatokea hasa kwa upande wa biashara za silaha.

Aidha, ameomba vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na nchi za Marekani na Muungano wa Ulaya dhidi ya serikali ya Syria visimamishwe kutokana na mahitaji ya kibinadamu nchini humo.

Amesema, serikali ya Syria iko tayari kufikia makubaliano ya kisiasa na upinzani, iwapo upinzani huo utawakilisha Wasyria wala si serikali za nje, na utapinga ugaidi.