Hali ya haki za binadamu Eritrea yatia shaka: Mtaalamu

29 Septemba 2014

Ukiukwaji wa kupindukia wa haki za binadamu nchini Eritrea ni moja ya shinikizo la raia wake kukimbia nchi hiyo kusaka maisha bora ughaibuni, ameonya mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hail ya haki za binadamu huko Eritrea Sheila B. Keetharuth.

Ametoa onyo hilo mwishoni mwa ziara yake ya siku tano nchini Italia ambako alikwenda kushuhudia mwenyewe hali halisi ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Ertirea.

Bi. Keetharuth amesema wengi aliozungumza nao wamesema waliwaili Italia baada ya safari ndefu yenye masahibu baharini na jangwani lakini wanaona ni vyema kuweka maisha yao rehani ili kupata hifadhi kwenye maeneo ambayo haki za binadamu zinaheshimiwa.

Amesema hadi mwezi huu wa Septemba, Italia imepokea wakimbizi wapya 135,000 ambapo kati yao 32,000 wanatoka Eritrea.

Mtaalamu huyo amesema raia hao wanakimbia kile alichosema ni mfumo wa aina yake wa kukiuka haki za binadamu ikiwemo udhibiti wa kisiasa, mauaji kinyume cha sheria, mateso na kufungwa katika magereza yasiyokidhi viwango vya kimataifa.

Amesema ni matumaini yake tume iliyoundwa kuchunguza haki za binadamu Eritrea itachunguza vitendo hivyo na kuweka fursa ya kuwajibika kwa wakosaji.

Ametaka serikali ya Eritrea, wananchi na jamii ya kimataifa kuipatia ushirikiano tume hiyo ili kupata ukweli halisi.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter