Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC yapanga muda wa kuthibitisha ndivyo au sivyo tuhuma dhidi ya Goudé

Charles Biblia Goudé wakati wa ufunguzi wa uthibitisho wa mashtaka juu yake Septemba 29, 2014 katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai katika Hague (Uholanzi) © ICC-CPI

ICC yapanga muda wa kuthibitisha ndivyo au sivyo tuhuma dhidi ya Goudé

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC imetangaza kuwa hatma juu ya iwapo Charles Blé Goudé wa Cote D’Ivoire atafunguliwa kesi au la itafahamika tarehe Pili mwezi ujao ambapo jopo tangulizi la majaji litakutana kusikiliza tuhuma hizo.

Uamuzi huo umefikiwa tarehe 29 Septemba baada ya mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda kuwasilisha taarifa zake katika kikao cha kuthibitisha mashtaka dhidi ya Goudé , sambamba na taarifa ya Paolina Massida ambaye ni wakili wa wahanga wa vitendo vinavyodaiwa kutekelezwa na mtuhumiwa.

Baada ya kusikilizwa kwa taarifa hizo, iliamuliwa kuwa tuhuma ziwe zimesikilizwa hadi tarehe Pili Oktoba mbele ya jopo tangulizi la majaji watatu likiongozwa na Silvia Fernández de Gurmendi. Majaji wengine ni Ekaterina Trendafilova na Christine van den Wyngaert.

Charles Blé Goudé anatuhumiwa kuwajibika yeye binafsi na kuwa mshirika wa makosa manne ya uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo mauaji, ubakaji na aina nyingine ya ukatili wa kingono, utesaji anayodaiwa kutekeleza huko Côte d’Ivoire kati ya tarehe 16 Disemba 2010 na 12 Aprili 2011.

Iwapo tuhuma zitathibitishwa, kesi itaanza kusikilizwa mbele ya jopo kamili la majaji.