Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utalii ulenge kuwezesha watu kiuchumi: Ban

Utalii ulenge kuwezesha watu kiuchumi: Ban

Kubaini na kutumia ipasavyo maslahi ya utalii itakuwa jambo muhimu katika kufikia ajenda ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015, ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon kwenye ujumbe wake wa siku ya utalii duniani Septemba 27.

Ban amesema ni kwa mantiki hiyo ndiyo maana maudhui ya siku ya utalii mwaka huu yanaangazia uwezo wa utalii katika kuinua uwezo wa watu kiuchumi na kijamii.

Amesema kitendo cha kushirikisha wananchi wa eneo husika lenye vivutio vya utalii kinaongeza uthabiti wa nchi hizo sambamba na kuziwezesha kuwa thabiti hata wakati wa majanga.

Mathalani Katibu Mkuu amesema utalii unasaidia watu kuendeleza stadi zao mbali mbali iwe kwenye kilimo, usanii, ujenzi na hata kupanua fursa za biashara.

Hivyo Ban ametaka serikali, wananchi kutumia siku ya leo kujizatiti kwa kutunga sera za utalii zenye maslahi kwa jamii zote.

Naye Katibu Mkuu wa Shirika la utalii duniani, UNWTO Taleb Rifai ametaka ujumbe wa mwaka huu Utalii na maendeleo ya jamii utumike kuimarisha jamii ambazo kwazo shughuli za utalii zinafanyika.