Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awa na mazungumzo na Waziri Lavrov wa Urusi

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon(kulia) akiwa na Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya kigeni wa Urusi. (Picha:Eskinder Debebe)

Ban awa na mazungumzo na Waziri Lavrov wa Urusi

Suala la Ukraine limekuwa moja ya ajenda ya mazungumzo kati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov, mazungumzo yaliyofanyika kando ya mjadala mkuu wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, siku ya Jumamosi.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema wakati wa mazungumzo hayo, Ban ameisihi Urusi kutumia ushawishi wake kuhakikisha kunapatikana makubaliano endelevu ya kusitisha mapigano akimjulisha Waziri Lavrov kuwa yeye binafsi anaendelea kushirikiana na viongozi wa dunia kusaka suluhu la amani la mzozo wa Ukraine.

Wawili hao pia wamejadili masuala mengine ikiwemo Syria ambapo wamekubaliana umuhimu wa kuwa na suluhu la dhati la kisiasa kuhusu Syria huku Ban akiiomba Urusi kuongeza kiwango chake cha mawasiliano na pande muhimu kwenye mzozo huo ili umalizike.

Kuhusu suala la nyuklia la Iran, Ban na Lavrov wamekubaliana kuwa kuna umuhimu wa kuwepo kwa mazungumzo yanayozingatia hali halisi.

Wamejadili pia rasi ya Korea ambapo Katibu Mkuu ameiomba Urusi kujihusisha na suala hilo ili kumaliza mvutano uliopo