Mamlaka ya UNMISS iangaliwe upya, mzozo wetu ni wa kisiasa si kikabila:Kiir

27 Septemba 2014

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amehutubia mjadala mkuu wa wazi wa mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York ambapo ameomba baraza la usalama liangalie upya mamlaka ya ujumbe wa Umoja huo nchini mwake, UNMISS ili yakidhi maslahi ya wananchi wake.

Amesema wana wasiwasi na hali ya sasa kwani anachofahamu yeye chini ya mamlaka ya sasa UNMISS haisaidii shughuli zinazoombwa na taasisi za kitaifa, kijimbo na wadau wengine kuhusu masuala ya marekebisho ya sekta ya ulinzi, upokonyaji silaha na ujumushi wa wapiganaji kwenye jamii na hata maendeleo.

(Sauti ya Rais Kiir)

“Tunaliomba baraza la Usalama kuangalia upya uamuzi huu pindi watakapojadili kuongeza muda wa UNMISS mwezi Novemba mwaka 2014. Kwa misingi hiyo hiyo tunaomba pia UNMISS kushiri katika kupanga upya shughuli zake zinazohusiana na ulinzi wa raia ili zibadilike kutoka ulinzi wa raia kwa nadharia kwenda ulinzi kwa vitendo.”

Katika hotuba yake Rais Kiir alitamka bayana kuwa mzozo wa nchi yake si wa kikabila bali kisiasa, na mwandishi wetu alizungumza naye ili afafanue.

(Sauti ya Rais Kiir)

“Natoka kabila la dinka, na Riek Machar aliyeongoza mapinduzi anatoka kabila la Nuer. Aliposhindwa mapinduzi, akabadili mwelekeo na kusema ni mzozo wa kikabila badala ya kusema kuwa alikuwa anataka kuchukua madaraka kwa njia ya mapinduzi, na aliposhindwa akabadili mwelekeo.”

Na kuhusu utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia, Rais Kiir amesema kwa sasa siyo kipaumbele.

(Sauti ya Rais Kiir)

“Vita na maendeleo haviendi pamoja. Kwa hiyo kipaumbele sasa ni kuleta amani ili kuweka hakikisho la miradi ya maendeleo ambayo tunataka kutekeleza. Kwa hiyo ni lazima tuache mapigano ndiyo tuweze kuzungumzia maendeleo thabiti.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter