IMF yaridhia dola Milioni 130 kudhibiti Ebola Sierra Leone, Liberia na Guinea

26 Septemba 2014

Shirika la fedha duniani, IMF limeidhinisha dola Milioni 130 kwa ajili ya kupambana na mlipuko wa Ebola kwenye nchi tatu za Afrika Magharibi wakati huu ambapo idadi ya watu waliokufa kutokana na ugonjwa huo imefikia karibu Elfu Tatu huku walioambukizwa ni zaidi ya Elfu Sita.

Bodi tendaji ya IMF ilifikia uamuzi huo siku ya Ijumaa ambapo mchanganuo wa fedha hizo unaonyesha kuwa Guinea itapatiwa dola Milini 41, Liberia dola Milioni 49 million ilhali Sierra Leone itapata dola Milioni 40.

Mkurugenzi Mtendaji wa IMF Christine Lagarde anafafanua..

"Kirusi cha Ebola kinasababisha siyo tu madhara ya kibinadamu huko Sierra Leone, Guinea na Liberia lakini pia madhara ya kiuchumi. Kwa hiyo nchi hizi tatu zimeomba msaada na tumeidhinisha dola Milioni 130 ambazo zitatumika kusaidia bajeti ya nchi hizo tatu. Kwa kweli wanahitaji kutumia fedha hizo kukabiliana na madhara yatokanayo na kirusi hicho cha Ebola.”

IMF inasema jangahilobado linazidi kuibuka lakini makadirio ya awali yanadokeza kuwa ukuaji wa uchumi mwaka huu huko Liberia na Sierra Leone utapungua angalau kwa asilimia Tatu hadi Tatu na nusu, ilhali huko Guinea utapungua kwa asilimia Moja na Nusu.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter