Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siri ya Tanzania kutimiza lengo namba nne la Milenia yawekwa bayana

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Radio ya Umoja wa Mataifa. (Picha: UN/Idhaa ya Kiswahili)

Siri ya Tanzania kutimiza lengo namba nne la Milenia yawekwa bayana

Mjadala Mkuu wa mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ulioanza tarehe 24  Septemba mwaka 2014 umetoa fursa kwa viongozi wa nchi na serikali kuhutubia na kuelezea mambo muhimu ya kitaifa na kimataifa yanayohusiana na utekelezaji wa misingi ya Umoja wa Mataifa ambayo ni pamoja na amani, maendeleo na haki za binadamu.

Miongoni mwa viongozi waliohutubia ni Rais Jakaya Kikwete ambaye aligusia amani na usalama duniani, maendeleo, uchumi na afya ikiwemo ugonjwa wa Ebola.

Mara baada ya hotuba yake, Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio ya Umoja wa Mataifa alipata fursa ya kuzungumza na Rais Kikwete ili afafanue mambo kadhaa ikiwemo vifo vya watoto wachanga na kauli yake ya kwamba Afrika si nchi moja yenye mikoa 54 bali ni bara lenye nchi huru 54.