Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukitaka kuweka historia, tutokomeze silaha za nyuklia- Kutesa

UN Photo/Devra Berkowitz
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Sam Kutesa,(

Tukitaka kuweka historia, tutokomeze silaha za nyuklia- Kutesa

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Sam Kutesa, amesema kuwa ikiwa ulimwengu unataka kuweka historia, ni lazima utokomeze silaha za nyuklia na kuzifanya kuwa jambo la hisoria.

Akiwahutubia mawaziri wawakilishi wa nchi wanachama katika halfa ya kuadhimisha Siku ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia kabisa, Bwana Kutesa amesema kuwa uwezekano wa majanga makubwa ya athari za matumizi ya silaha za nyuklia popote pale kwenye sayari dunia ni ukumbusho wa haja ya kufanya juhudi za haraka na kwa bidii kupinga na kutokomeza silaha hizo kabisa.

“Siku hii ni fursa ya kuongeza uelewa na elimu ya umma kuhusu hatari inayoletwa kwetu wanadamu na silaha za nyuklia. Pia ni fursa ya kuchagiza juhudi zaidi za kimataifa ili kufikia lengo la pamoja la ulimwengu usio na silaha za nyuklia. Kama rais wa Baraza Kuu, nina furaha kujumuika katika maadhimisho haya, na lengo la kuwa na ulimwengu usio na silaha za nyuklia, ambalo ni muhimu kwa kufikia amani na usalama wa kimataifa.”

Bwana Kutesa amesema athari za kulipuliwa silaha za nyuklia, iwe kwa ajali, kutolenga vyema au kwa kukusudia, zinaweza kuwa zenye madhara makubwa.

“Juhudi zote zielekezwe kwa kulitokomeza tishio hili. Leo tuna fursa ya aina yake kuzungumza kwa kauli moja: ‘ukitaka kuweka historia, zifanye silaha za nyuklia kuwa historia.’”