Mvua na usafiri zakumba ufikishaji misaada ya WFP CAR

26 Septemba 2014

Shirika la Mpango wa Chakula duniani, WFP limetangaza kufanikiwa kufikisha misaada ya chakula kwa watu 400,000 nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR idadi hii ikiwa ni sawa na asilimia 10 ya idadi ya watu wote nchini humo. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, msemaji wa WFP, Elizabeth Byrs amesema operesheni zao CAR zinakabiliwa na matatizo mawili makubwa:

Ukosefu wa usalama unaongezela hasa katikati ya nchi na kaskazini, kwenye maeneo ya Ouam, na pia usafirishaji wa vifaa, yaani tuko bado kwenye msimu wa mvua, utakaoendelea hadi mwezi Disemba, barabara ni mbaya sana, malori yanaanguka, madaraja yanaharibika, na malori yakianguka, yanaporwa”

Hata hivyo, amesema, WFP imefanikiwa kufikisha tani 4800 za vyakula kwa watu 400,000, kwa kupitia njia mbalimbail zikiwemo boti kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, malori na ndege.

Aidha Elizabeth Byrs ameshukuru pia Urusi kwa kutoa msaada wa malori 40 aina ya KAMAZ ambayo kwa mujibu wake, ni malori imara zaidi duniani yanayostahamili hali ngumu ya barabara kama ilivyo sasa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter