Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo dhidi ya Ebola penginepo Januari mwakani:WHO

Picha: WHO/N. Alexander

Chanjo dhidi ya Ebola penginepo Januari mwakani:WHO

Shirika la afya duniani, WHO limesema nchi za Afrika Magharibi zilizokumbwa na Ebola zitalazimika kusubiri zaidi kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo kwani ni lazima zile mbili za sasa zinazofanyiwa majaribio zithibitike kuwa ni salama kwa binadamu. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

WHO imesema hayo ikiongeza kuwa tafiti zinaendelea ili kubaini iwapo damu na plasma kutoka kwa mgonjwa aliyepona Ebola vinafaa kutibu wagonjwa wa Ebola.

Dkt. Marie Paule Kieny wa WHO amesema ijapokuwa kuna wagonjwa waliopona baada ya kupatiwa damu hiyo, bado kuna maswali kuhusu usalama na uthabiti wake pamoja na utekelezaji wake kwenye nchi ambazo tayari mifumo ya afya imeporomoka na uhaba wa wahudumu wa afya.

(Sauti ya Dkt. Kieny)

“Tunaweza kuanza kutumia baadhi ya hizi chanjo kwenye nchi zenye mlipuko kuanzia Januari mwakani. Lakini hii haitakuwa kampeni kubwa ya chanjo, bora tuweke bayana kwa sababu idadi ya chanjo itakayopatikana haitawezesha hili. Wiki ijayo tutajadiliana na wataalamu juu ya nani anapaswa kuwa mtu wa kwanza kupatiwa chanjo hii. Na hii itafanyika baada ya mtu kuwa ameelimishwa. Chanjo hii hazitakuwa zimepatiwa leseni, kwani hii ni sehemu ya uamuzi wa kibinadamu ulioelezwa na kujadiliwa kwenye mkutano wa WHO.”

Hadi sasa Ebola imekumba watu zaidi ya 6,200 huko Guinea, Liberia na Sierra Leone ambapo kati yao hao takribani 3,000 wamefariki dunia wakiwemo pia wahudumu wa afya.