Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaonya kuhusu kuongezeka kwa wakimbizi na waomba hifadhi ugenini

UNHCR yaonya kuhusu kuongezeka kwa wakimbizi na waomba hifadhi ugenini

Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR,  inaonyesha kuwa idadi ya watu wanotafuta hifadhi kama wakimbizi katika nchi zilizoendelea ilizidi kupanda katika nusu ya kwanza ya mwaka 2014, sababu kubwa ikiwa ni vita nchini  Syria na Iraq sawa na migogoro na hali ya ukosefu wa utulivu Afghnaistan, Eritrea na kwingineko.

Ripoti hiyo mpya ya UNHCR kuhusu mwelekeo wa usakaji wa hiafdhi, ambayo msingi wake ni taarifa zilizopokelewa kutoka serikali 44  Ulaya, Amerika ya Kaskazini na maeneo ya Asia -Pasifiki, inasema watu 330,700 waliomba hifadhi kama wakimbizi katika nchi hizi kati ya mwanzo wa mwezi Januari na mwisho wa mwezi Juni, hili likiwa ongezeko la asilimia 24 kuliko nusu ya pili ya mwaka jana ambapo watu 328,100 waliomba hifadhi.

Ripoti hiyo inaonya kuwa, kulingana na historia ya idadi kubwa ya watu walioomba hifadhi katika nusu ya pili ya kila mwaka, waomba hifadhi mwaka wa 2014 wataweza kufikia watu 700,000- hiki kikiwa ni kiasi cha  juu zaidi katika nchi zilizoendelea katika miaka 20,  kiwango ambacho hakijawahi konenekana tangu  migogoro ya  miaka ya 1990 Yugoslavia ya zamani .

Kamishna Mkuu wa UNHCR, Antonio Guterres amesema, ni wazi tuko katika zama za kuongezeka kwa migogoro, na mfumo wa kimataifa wa kibinadamu tayari upo katika shida kubwa .

Aidha Guterres ameongeza kuwa, jumuiya ya kimataifa inahitaji kuandaa raia wao kuwa iwapo hapatakuwa na ufumbuzi kwa migogoro, katika miezi na miaka ya hivi karibuni watu wengi watakuwa wakimbizi  na watahitaji huduma.