Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhalifu Sudan Kusini utapaswa kukabiliwa na sheria ya kimataifa: Ban

UN photos - Stuart Price
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa mjini Abyei, Mei 2014. Picha ya

Uhalifu Sudan Kusini utapaswa kukabiliwa na sheria ya kimataifa: Ban

Mkutano maalum umefanyika siku ya Alhamis tarehe 25 Septemba kuhusu Sudan Kusini wakati wa kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akisema kwamba watoto 50,000 wako hatarini ya kufa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Amesikitishwa kuona kwamba taifa hilo changa kabisa duniani linafilisika wakati lina fursa zote za kuwa na maendeleo mazuri ya kiuchumi, yakiwemo akiba za mafuta na udongo mzuri kwa kilimo.

Akishukuru wafadhili na nchi zinazotuma walinda amani, amewaomba kuongeza misaada yao akieleza kwamba Umoja wa Mataifa unatarajia kuongeza walinda amani 5,000 katika ujumbe wa Umoja huo Sudan Kusini, UNMISS, ukiwa ni ujumbe mkubwa zaidi katika historia ya Umoja wa Mataifa.

Hatimaye, ametoa wito kwa viongozi wa Sudan Kusini, akisema pia kwamba uhalifu uliotekelezwa nchini humo utapaswa kukabiliwa kisheria katika kiwango cha kimataifa.

(Sauti ya Ban)

Nina ujumbe kwa viongozi wa Sudan Kusini. Mmefungua vidonda vilivyosababisha maumivu mengi, sasa mnapaswa kuvitibu. Mnapaswa kufanya hivi kwa ajili ya raia wenu na vizazi vitakavyokuja baadaye

Mkuu wa idara ya operesheni za kulinda amani katikaUmoja wa Mataifa, Herve Ladsous, naye amesema ingawa ilikuwa ni lazima kupokea wakimbizi ndani ya kambi ya UNMISS wakati wa mwanzo wa mapigano, hali si endelevu, kwani kambi za UNMISS hazikujengwa kwa ajili ya kupokea wakimbizi, akiongeza kwamba ni lazima kupata suluhu ya kudumu kwa wakimbizi hawa.

Kwa upande wake katibu mkuu wa Shirika la Madaktari bila mipaka Jerome Oberreit amesema ingawa mashirika ya kimataifa mengi yamejitahidi kutoa usaidizi kwa Sudan Kusini, msaada huo unapaswa kusambazwa hadi kwenye maeneo yanayofikika kwa taabu, na yaliyoathirika na utapiamlo na ukosefu wa huduma za afya.