DRC yataka Afrika ipewe kiti cha kudumu kwenye Baraza la Usalama

25 Septemba 2014

Ugaidi, Ebola na vitisho kwa usalama ni matatizo matatu makubwa yanayokumba dunia ya leo, kwa mujibu wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Joseph Kabila.

Katika hotuba yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,Kabiba ameiomba jamii ya kimataifa ijitahidi kupambana na ugaidi unaoathiri zaidi raia wa Afrika siku hizi.

Kuhusu mlipuko wa Ebola, amekaribisha usaidizi wa jamii ya kimataifa uliokuja wakati ugonjwa huo ukagunduliwa kama tishio kwa dunia nzima, si tu kwa raia wa Afrika. Amechukua nafasi hiyo kutangaza kuundwa kwa chuo maalum cha mafunzo nchini DRC kuhusu magonjwa yanayoambukizwa zaidi, kutokana naa uzoefu wa DRC juu ya masuala hayo.

Halikadhalika amerudia msimamo wa DRC kusaidia katika kuhakikisha kuwepo kwa amani duniani na hasa katika bara la Afrika, akikumbusha kwamba imechangia kwa kutuma wanajeshi wake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Amesisitiza kuwa bila amani hakuna maendeleo, akitoa mfano wa nchi yake inayoendelea kuimarisha hali ya amani, wakati uchumi unazidi kuwa kwa kasi kubwa na miundombinu zinaendelea kujengwa.

Hatimaye, amerudia wito wake kuwa Afrika iwakilishwe ipasavyo katika mamlaka za Umoja wa Mataifa, hasa katika Baraza la Usalama, akisema:

(Sauti ya Kabila)

Siyo sawa, wakati nchi sita kati ya nchi kumi zinazokuwa kwa kasi kubwa duniani kiuchumi ziko Afrika, wakati Afrika inakuwa na nguvu zaidi kutokana na ukuaji wa uchumi wake na ongezeko la idadi ya watu wake, wakati akiba zake za maji, misitu na udongo wa kilimo ni muhimu sana katika kujenga maendeleo endelevu, siyo sawa kuwa bara la Afrika halina kiti cha kudumu katika chombo cha Umoja wetu chenye jukumu la kuangazia usalama na amani duniani. Tumechelewa, na muda umefika sasa wa kuona mabadiliko

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter