Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutokomeza njaa kunawezekana : WFP na IFAD

Picha ya WFP

Kutokomeza njaa kunawezekana : WFP na IFAD

Viongozi wa dunia wamekutana Alhamisi mjini New York kujadili jinsi ya kutokomeza njaa duniani kote, wakitoa mifano thabiti ya hatua nchi zilizochukuliwa na nchi zao kufikia azma hiyo.

Lengo la mkutano huu ulikuwa ni kuonyesha matokeo katika Mchakato wa Kutokomeza Njaa uliozinduliwa mwaka 2012 na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.

Akizungumza kwenye mkutano huo kwa niaba ya Ban, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la mpango wa chakula duniani, Ertharin Cousin, amesema mafanikio mengi yamepatikana katika kufikia lengo namba moja la malengo ya maendelo ya milenia ikiwemo nchi 63 kufanikiwa kupunguza kwa asilimia 50 idadi ya watu walioathirika na njaa.

Hata hivyo, amesema, changamoto bado zipo,

(Sauti ya Ertharin)

“ Mtu mmoja kati ya tisa bado anakumbwa na njaa kila siku, Ongezeko la idadi ya watu, mabadiliko ya tabianchi, pamoja na mizozo ya vita na ya afya zinachangia kuleta dharura katika kazi zetu. Tunawajibika kwa watu milioni 805 wanaoathirika na njaa. Tunaweza kutimiza ahadi yetu ya kutokomeza njaa”

Washiriki wa mjadala huo wamezingatia umuhimu wa kubaini njia mbadala ya kuwasaidia watu kupata vyakula vyenye lishe bora, pamoja na kuwezesha wakulima wadogo wadogo, kwa kuwapatia mbegu bora na kuimarisha uzalishaji wa udongo.

Kwa upande wake mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo IFAD, Kanayo F. Nwanze amesema hatuwezi kuacha watu zaidi ya milioni 800 kulala njaa kila siku wakati kuna uwezo wa kulisha watu wote duniani.