Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bahari ni muhimu kwa tabianchi yetu- FAO

UN Photo/Stuart Price
Bahari. Picha@

Bahari ni muhimu kwa tabianchi yetu- FAO

Udhibiti bora wa rasilmali za bahari duniani ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula duniani, amesema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo, FAO, José Graziano da Silva, wakati wa mjadala uliofanywa kwenye Umoja wa Mataifa leo, ukimshirikisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry.

Mjadala huo umeandaliwa kufuatia mkutano wa tabianchi ulioafanyika wiki hii, na umelenga kudakia nafasi ya uwepo wa viongozi wa kimataifa waliokuja kwenye mkutano wa Baraza Kuu ili kumulika mabahari na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha uvuvi endelevu na ulinzi wa maeneo ya maji.

Bwana Graziano da Silva amewaambia washiriki kwenye mjadala huo kuwa asilimia kumi ya watu kote duniani wanategemea uvuvi kwa riziki zao, na watu wapatao bilioni 4.3 hutegemea samaki kwa asilimia 15 ya lishe ya protini.

Waziri John Kerry amesema juhudi bora zinahitajika katika ulinzi wa idadi ya samaki katika mabahari, ambao huchangia pakubwa kwa uchumi wa mamilioni ya familia na usalama wa chakula kwa mamilioni ya watu.