Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Benki ya Dunia yatoa dola Milioni 400 kusaidia Ebola; Liberia yasema ugonjwa umewapiga butwaa

Photo © Francis Ato Brown/World Bank

Benki ya Dunia yatoa dola Milioni 400 kusaidia Ebola; Liberia yasema ugonjwa umewapiga butwaa

Benki ya dunia imetoa dola Milioni 400 kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola huko Afrika Magharibi.

Tangazo hilo limetolewa na Rais wa Benki ya dunia, Dkt. Jim Yong Kim wakati akihutubia mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Ebola kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

(Sauti ya Dkt. Kim)

Siku tisa zilizopita tuliidhinisha dola Milioni 105, tayari tumeshazipeleka, na yeyote anayefanya Benki ya dunia anatambua kuwa hayo ni maajabu. Lakini nilirudi tena kwa Bodi ya wakurugenzi na kuwasihi tuongeze maradufu mchango wetu kwa hiyo sasa tutakuwa tumechangia dola Milioni 400.

Akihutubia kwa njia ya Video kutoka Monrovia, Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia amesema ugonjwa wa Ebola umepora jamii mfumo wao wa maisha ya kila siku na kuwaacha wamepigwa na butwaa mathalani kushuhudia maiti za wapendwa wao zikichukuliwa na watu wasiowafahamu na hata kushindwa kutoa buriani. Hata hivyo akasema hawakati tamaa.

(Sauti ya Rais Ellen)

Tunapambana. Kutokana na msaada wa wengi wenu, tunaimarisha harakati zetu kwa kujenga na kuimarisha vituo vya afya na matibabu nchini kote. Tunazuia maambukizi kwa kutoa elimu kwa umma ili kubadili tabia.”