Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola:Ugonjwa unaua watu 200 kila siku, Ban atoa pendekezo.

Picha: UNICEF Sierra Leone/2014/Dunlop

Ebola:Ugonjwa unaua watu 200 kila siku, Ban atoa pendekezo.

Mkutano wa ngazi ya juu kuhusu ugonjwa wa Ebola ambao hadi sasa  umeua watu zaidi ya 2800 huko Afrika Magharibi, umefanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, huku shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF likitangaza kuwasili kwa vifaa tiba muhimu kwenye mji mkuu wa Liberia, Monrovia. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Mkutano huo ukiangazia hatua za kimataifa za kudhibiti Ebola, umeitishwa na Katibu Mkuu Ban Ki-Moon ambapo ameeleza bayana kuwa hali ni mbaya hivi sasa kwani ugonjwa unaua watu 200 kila siku huko Afrika Magharibi.

Ban amesema hatua za usaidizi zimechukuliwa ikiwemo kutuma wahudumu na vifaa lakini akatoa pendekezo.

“Janga limeangazia umuhimu wa kuimarisha mifumo ya utambuzi na kuchukua hatua. Tunapaswa kuangalia iwapo dunia inahitaji kuunda jopo la wataala, wa afya wanaosubiri kuchukua hatua iwapo janga linatokea, likipatiwa usaidizi wa WHO na kuwezeshwa na Umoja wa Mataifa. Kama ilivyo walinda amani wanasaidia ulinzi, basi na wahudumu wa afya wanaweza kulinda afya za watu.”

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Margaret Chan akasema hali itakuwa mbaya sana kabla ya kuwa nzuri hivyo akataka wakuu wa nchi wachukua hatua huku Rais Barack Obama wa Marekani amehutubia akisema kuwa hatua zisipochukuliwa mamia ya maelfu ya watu watapoteza maisha.

(sauti ya Obama)

“Ikiwa kuna hali yoyote ya dharura ya afya ya umma, inayohitaji kukabiliwa kwa njia mathubuti na haraka, kimataifa, ndio hii.”